Jumamosi , 24th Mar , 2018

Mchezaji wa bora wa dunia Cristiano Ronaldo usiku wa kuamkia leo amefanikiwa kuonesha ubabe wake mbele ya nyota wa Misri, anayefanya vizuri kwasasa na klabu yake ya Liverpool Mohamed Salah baada ya kuisawazisha Ureno na kufunga bao la ushindi.

Ronaldo ameonesha umwamba huo kwenye mechi ya kirafiki ya kalenda ya FIFA ambapo timu yake ya Ureno ilikuwa mwenyeji wa Misri na ilikubali kuwa nyuma kwa bao la Salah hadi dakika ya 90 kabla ya Ronaldo kubadili mambo.

Salah aliitanguliza Misri kwa bao la dakika ya 56 kisha Ronaldo kuamua ushindi wa mabao 2-1 kwa timu yake ya Ureno kwa mabao ya dakika ya 90+2 na 90+4.

Baada ya mabao hayo mawili Ronaldo sasa amefikisha jumla ya mabao 81 ya kuifungia timu yake ya taifa akiwa ndio mchezaji mwenye mabao mengi zaidi akifuatiwa na Messi mwenye mabao 61 aliyoifungia Argentina.

Mohamed Salah kwasasa ndio anaongoza mbio za ufungaji bora kwenye ligi kuu soka ya England akiwa na mabao 28, wakati Ronaldo ana mabao 22 kwenye ligi kuu ya soka Hispania.