Jumatatu , 24th Sep , 2018

Uongozi wa klabu ya Yanga umekanusha uwepo wa taarifa za majeraha ya mshambuliaji wake, Heritier Makambo kufuatia kutopangwa katika mchezo dhidi ya Singida United wikiendi iliyopita.

Mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo.

Mshambuliaji huyo hakupangwa katika listi ya kikosi cha kwanza cha mchezo huo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa 2-0, kulikopelekea kuzuka kwa taarifa juu ya majeraha yake na kuwa anaweza kukosekana katika mchezo dhidi ya watani wao wa jadi Simba utakaopigwa wikiendi hii.

Akizungumza na www.eatv.tv juu ya ukweli wa taarifa hiyo , Afisa habari wa Yanga, Dismas Ten amesema,

"Ni kweli Makambo hakucheza na si lazima acheze mechi zote, kiujumla yuko vizuri hana tatizo lolote na anafanya mazoezi kama kawaida", amesema Ten.

"Kucheza na kupumzika kwa mchezaji ni jambo la kawaida tuu kwasababu yeye naye ni binadamu kama wengine ambao huwa wakichoka wanapumzika hawafanyi kazi. Na kwenye hili wala asisemwe kocha kwasababu hiyo ni kawaida,  hata waliocheza jana ni wachezaji wa Yanga, yeye atacheza kwenye michezo inayofuata ", ameongeza Dismas.

Yanga itapambana na watani wao Simba, 30 Septemba katika ligi kuu Tanzania bara, mchezo ambao tayari umekwishaanza kuzua gumzo miongoni mwa mashabiki wa soka hasa wa timu hizo.

Ushindani mkubwa katika mchezo huo unatarajiwa kuwa katika kuwania nafasi ya kwanza ya msimamo wa ligi ambapo mpaka sasa Yanga inaongoza kwa alama 12 katika michezo yake minne huku Simba ikiwa katika nafasi ya tatu kwa alama zake 10 baada ya kushuka dimbani mara tano.