Ijumaa , 25th Mei , 2018

Daktari wa timu ya Liverpool, Ruben Pons amesema kwamba mshambuliaji Mohamed Salah hatashiriki mfungo wa mwezi wa Ramadhan kwa siku mbili kuelekea mchezo wa fainali wa klabu bingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid.

Daktari huyo amesema hayo leo Mei 25, 2018 wakati akihojiwa na kituo cha radio Cadena SER na kuongeza kuwa katika siku ya Ijumaaa na Jumamosi mchezaji huyo hatashiriki mfungo wa Ramadhan na haitakuwa na madhara yoyote kwa mchezaji huyo.

Taarifa hiyo inakuja baada ya kuenea uvumi kwamba mshambuliaji huyo ataendelea na mfungo wa Ramadhan hata katika siku ya mchezo wa fainali dhidi ya Real Madrid.

Mshambuliaji huyo raia wa Misri ambaye ni muumini wa dini ya kiislamu amekuwa na mafanikio katika klabu ya Liverpool baada ya kufanikiwa kupachika magoli 44 katika michuano yote msimu huu.

Katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan waumini wa dini ya kiislamu wanapaswa kufunga kula na kunywa katika kipindi cha mchana mpaka jioni, hivyo ilipekea kuweka shaka kwa wapenzi wa soka kuona Salah atashiriki vipi mchezo wa fainali akiwa katika mfungo.

Liverpool na Real Madrid zitakutana kesho Mei 26, 2018 katika mchezo wa fainali wa ligi ya mabingwa ulaya katika mji wa Kiev nchini Ukraine.