Jumamosi , 24th Mar , 2018

Nyota wa Tanzania Mbwana Samatta anayekipiga kwenye klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji amesema anaimani kubwa kwamba Simon Msuva anayechezea klabu ya Difaa El Jadidi atafanya vizuri katika ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na uzoefu aliokuwa nao kwa sasa.

Samatta ametoa kauli hiyo kufuatia hatua ya makundi ya mashindano ya Mabingwa Afrika kupangwa ambapo timu anayochezea Winga Simon Msuva kuangukia kundi B ikiwa pamoja na timu ya TP Mazembe, Mouloudia Club D’alger pamoja na ES Setifienne.

"Nimeangalia makundi yote lakini inaonekana kundi lao ndio lenye uzito na kuna mtu nilimwambia hili kundi ambalo wamepangwa kina Msuva sio jepesi lakini kwa sasa Msuva ana uzoefu wa pande zote mbili kwa sababu anacheza katika nchi ya kiarabu kwa hiyo amezoea hali ya soka la kiarabu. Tayari ameshacheza na  AS Vita ya DRC Congo kabla ya hawajaingia kwenye hatua ya makundi na ameshacheza sana Afrika kwa hiyo anafahamu nini kinachotakiwa katika soka la Afrika", amesema Samatta.

Pamoja na hayo, Mbwana Samatta ameendelea kwa kusema "naimani atafanya vizuri kwa sababu kama aliweza kufanya vizuri kwenye mechi ya AS Vita na TP Mazembe basi hata sasa atafanya zaidi pia na kwa timu yake ninavyoiona na mwenendo wao wanaweza kuvuka kwenye hilo kundi".

Kwa upande mwingine, Samatta amesema anatumaini kubwa juu ya Simon Msuva kufanya vizuri katika michuano hiyo kwasababu kwa sasa ameweza kuimudu hali ya hewa ya ubaridi.