Alhamisi , 17th Jun , 2021

Mlinzi mzoefu wa Sergio Ramos ametoa maelezo juu ya ni kipi kimesababisha aondoke katika klabu hiyo ikiwa ni baada ya miaka 16 ya mafanikio tangu ajiunge na wababe hao wa soka ngazi ya vilabu.

Nahodha wa zamani wa Real Madrid, Sergio Ramos(Pichani) enzi zake akiwatumikia mabingwa wa kihistoria wa Ulaya ngazi ya vilabu.

Ramos amesema haya;

''Real Madrid walitaka kunipa mkataba mpya nami nilikubaliana nao, ukiwa na kipengele cha kupunguza mshahara kwa 10%

na sikuwa na pingamizi kwenye ombi hilo kwakuwa pesa haikuwa kipaumbele changu, nami nikawaomba mkataba wa miaka miwili''.

''Kwa bahati mbaya sana klabu iligoma kusikiliza wao walitaka wanipe mwaka mmoja pekee, sikujisikia vizuri kwenye hilo, nilitazama namna nimepambania klabu, haikuwa kama upendeleo bali nilistahili mkataba wa miaka miwili''.

''Lakini kwa mapenzi yangu kwa hii klabu nikawaomba nikaifakari ofa ya mwaka mmoja walionipa kisha nitarejea.Baada ya tafakuri nilirejea baada ya muda kupita, nikawaambia nipo tayari kukatwa mshahara na kusaini huo mwaka mmoja,majibu niliyopewa ni kuwa, muda wa kusaini huo mkataba ulishapita hivyo nitafute timu ya kucheza''.

''Binafsi wakati tunaachana kwa mara ya kwanza kwenda kutafakari hawakuniambia kama kuna muda maalum, bali nikiwa tayari nikasaini.Tayari yameshatokea, siondoki Madrid kisa pesa bali sikupewa mkataba mpya.''.

Ramos ameagwa rasmi leo akiwa na takwimu nzuri za kujivunia ikiwemo kutwaa mataji 22, kufunga mabao 101 na asisti 40 katika michezo 671 aliyoitumikia Real Madrid.