Jumanne , 25th Feb , 2020

Aliyewahi kuwa Afisa Habari wa Yanga, ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amesema kuwa ameamua kurejea katika klabu hiyo kwa ajili ya kuendeleza mshikamano.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro

Amesema hayo kupitia mkutano ulioitishwa na uongozi wa klabu hiyo ukiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa klabu, Fredrick Mwakalebela, ambapo amesema kuwa amekuja kutoa sapoti yake kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Gwambina FC kesho.

"Nimekuja tena Yanga sikuitwa ila karaha na fedheha zimezidi nikaona nije tena tushirikiane. Potelea mbali ukuu wa Wilaya ulinikuta nikiwa Yanga hivyo nimeona nirudi na sijaja kuwa kiongozi ila lazima tuungane na kesho Gwambina hana pakutokea", amesema Jerry Muro.

"Mimi niliachia kijiti kwa kina Antonio Nugaz lakini upande wa Simba mwenzangu kakomalia hapo hapo sijui yeye ndio msukule wa Simba?. Kwetu sisi watu wanabadilika, walio walianza na Mo Dewji tangu akiwa mdogo mpaka leo wanamtegemea yeye tu, sisi wamepita kina Manji na wengine Yanga inasonga tu ndio tofauti yao na sisi", ameongeza.

Kuhusu kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, Mkuu huyo wa Wilaya amesema, "na mimi kama mwanachama huru nimwambie kocha tumemvumilia sana, kesho tunataka magoli 7, alitoka Ulaya huko kuja hapa atajua anafanyaje".

Aidha Jerry Muro ametoa wito kwa viongozi wote waliowahi kuhudumu klabuni hapo, kurudi na waendelee kuishi kama zamani, kuanzia kesho itakaposhuka dimbani dhidi ya Gwambina FC.