Jumatatu , 18th Feb , 2019

Kuelekea mchezo wa kesho ligi kuu soka Tanzania bara, Klabu ya soka ya Simba kupitia kwa kocha wake Patrick Aussems, amesema atawaacha nje ya kikosi baadhi ya wachezaji waliocheza dhidi ya Yanga.

Kikosi cha Simba

Akiongea jijini Arusha ambako utafanyika mchezo huo, Aussems ameeleza sababu ya kutowachezesha wachezaji hao ni kuwapa muda wa kupumzika kwaajili ya mchezo ujao dhidi ya Azam FC.

''Nina amini kesho tuitapata matokeo mazuri na mashabiki watafurahia, lakini nitafanya mabadiliko kwa kuwapumzisha baadhi ya wachezaji ambao walicheza mchezo uliopita ili wawe fiti zaidi kucheza mchezo ujao dhidi ya Azam'', amesema Aussems.

Kocha mkuu Patrick Aussems (kulia) na msaidizi wake Denis Kitambi

Simba inakabiliwa na ratiba ngumu ya kucheza mechi 4 ndani ya siku 12 na hiyo ni katika kupunguza viporo vyake kwenye ligi ili iweze kwenda sawa na vilabu vingine ambavyo vipo katika raundi ya 27 huku Simba wakiwa raundi ya 16.

African Lyon inashika nafasi ya mwisho kwenye ligi ikiwa na pointi 21 tu katika mechi 26 wakati Simba ipo nafasi ya 3 ikiwa na pointi 39 kwenye mechi 16.