"Simba waachane 'Maabara ya Kienyeji' " - Kindoki

Jumatatu , 13th Jul , 2020

Shabiki kindakindaki wa klabu ya Yanga, Jimmy Shomari maarufu kama 'Jimmy Kindoki' amesema Simba wanapaswa kuachana na masuala ya kienyeji kwakuwa wanakwenda kuwa wa Kimataifa msimu ujao.

Jimmy Kindoki

Amesema hayo baada ya timu yake kukubali kipigo cha mabao 4-1 hapo jana kutoka kwa mahasimu wao Simba kwenye mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) katika Uwanja wa Taifa.

Kindoki amesema wao kama Yanga wamekubali kipigo hicho lakini wanakitafakari na watakilipa msimu ujao, lakini akiwapa rai Simba kuachana na masuala ya kienyeji uwanjani kwani yamewafanya wachezaji wa Yanga kuchoka.

"Wametufanyia roho mbaya sana jana, wamenifanya nilale na vidonge. Nimechukia na nasema Simba mna roho mbaya sana na hii tutakuja kulipa kisasi", amesema.

"Jana kuna namna ambayo Simba wamefanya uwanjani tunaita 'Maabara ya Kienyeji', wamefanya vitu vikubwa sana pale uwanjani ndiyo maana wachezaji wetu walikuwa wazito. Simba imesajili vizuri na inakwenda kimataifa lakini bado wanaendekeza hayo mambo", ameongeza.

Baada ya mchezo huo, sasa Simba inafuzu hatua ya Fainali ya Kombe la Shirikisho ambapo itakutana na Namungo FC katika Uwanja wa Nelson Mandera mjini Sumbawanga katika mkoa wa Rukwa na kwa maana hiyo, Yanga imekosa nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.