Alhamisi , 9th Jan , 2020

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu amesema kuwa kwa sasa hawako tayari kuzungumzia juu ya uwezekano wa kukutana na Yanga katika fainali kabla ya mchezo wa nusu fainali.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu

Ameyasema hayo katika mkutano na wanahabari kisiwani Ugunja kuelekea mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Azam FC utakaopigwa kesho Januari 10.

Rweyemamu amesema kuwa kuizungumzia Yanga hivi sasa itakuwa ni kutoitendea haki game hii ya sasa ya nusu fainali iliyo mbele yao.

"Kwa bahati tumepata timu bora kwenye nusu fainali hii, kwa maana ya Simba, Yanga, Azam FC na Mtibwa Sugar. Fainali itakuwa nzuri kwa timu yoyote itakayovuka na sisi akili yetu yote tunaelekeza kwenye mchezo huu na baada ya hapo tutaizungumzia fainali dhidi ya Yanga", amesema Rweyemamu.

Kwa upande wa Azam FC ikiongozwa na Meneja wake Philip Alando, umesema kuwa wamejiandaa kwa ajili ya mchezo huo na mazoezi yao yako vizuri kuelekea mchezo.

Yanga inacheza na Mtibwa Sugar leo katika nusu fainali ya kwanza huku Simba ikitarajia kupambana na Azam FC hapo kesho na mchezo wa fainali ukitarajia kupigwa Januari 12.