Simba wajutia, Yanga kuwakosa nyota watatu

Jumatatu , 13th Mei , 2019

Kocha wa Simba Patrick Aussems, ameitupia lawama klabu ya Azam FC kuwa ilitumia muda mwingi kujiangusha kwa kuwa walikuwa wanatafuta sare huku akiweka wazi kuwa wamepata sare ambayo hawakustahili.

Emmanuel Okwi wa Simba na Aggrey Moris wa Azam FC

Aussems ameeleza kuwa wamecheza vizuri na kutawala mchezo hivyo walistahili ushindi lakini haijawa hivyo kutokana na Azam kujilinda zaidi.

"Walikuja kutafuta alama moja hivyo walikuwa wanapoteza muda, tulifanya mashambulizi mengi lakini hatukufanikiwa kufunga, tumepata alama moja lakini ambayo hatukustahili kwa namna tulivyotawala mchezo."- Aussems.

Baada ya mchezo wa leo wa Simba na Azam FC kumalizika kwa suluhu, kesho utapigwa mchezo mwingine wa ligi kuu kati ya Yanga dhidi ya JKT Tanzania.

Katika mchezo huo Yanga ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 80 kwenye mechi 35, itawakosa nyota wake Mohamed Banka, Gadiel Michael na Andrew Vicent ambao wote ni majeruhi.

Baada ya mechi ya leo Simba imeendelea kubaki kileleni ikiwa na pointi 82 kwenye mechi 33 wakati Azam FC wakibaki nafasi ya 3 na pointi 69 kwenye mechi 36.