Jumatatu , 11th Nov , 2019

Shirikisho la Soka Visiwani Zanzibar ZFF na Shirikisho la Soka Tanzania TFF zimekuwa katika mzozo katika siku za hivi karibuni kutokana na sababu mbalimbali, ambapo mzozo huo umeanza kuonesha dalili za kutatuliwa.

Shirikisho la Soka Tanzania na Shirikisho la Soka Zanzibar

Kwa mujibu wa Msemaji wa ZFF, Adam Abdallah Natepe kuthibitisha kuwa tayari kikao cha kwanza kimefanyika jana, Novemba 10 visiwani Zanzibar, ambapo ameeleza wamefikia mahali pazuri.

"Jana tumekaa kikao cha kwanza hapa Zanzibar baina yetu na TFF na tumefikia mahala pazuri, mkutano mwingine utafanyika Novemba 15 Jijini Dar es Salaam, jumla tutafanya mikutano kama minne hivi ukiwemo wa viongozi wa juu wa ZFF na TFF.", amesema Natepe

Aidha Natepe amesema kuwa wao kama ZFF hawana tatizo kubwa na TFF lakini wanachokihitaji ni ushirikiano mzuri katika masuala ya nchi, akitolea mfano 'program' za soka la wanawake, soka la vijana ambazo pesa zake hutolewa na FIFA.

Pia amesema suala lingine wanalolihitaji zaidi ni ushirikiano katika masuala mbalimbali yanayohusu timu ya taifa, tofauti na ilivyotafsirika kuwa wana mgogoro na TFF kutokana na kutokuwa na uwakilishi wa wachezaji wa Zanzibar katika timu ya taifa.

"Sisi hatusemi kuwa ni lazima wachezaji wetu waitwe Taifa Stars hapana, kocha ndiye anajua wachezaji gani wanamfaa na huo mfumo upo hata kwa wenzetu, lakini kocha anapochaguliwa anatakiwa kuja Zanzibar kuangalia ligi ya huku na vipaji vyake", ameeleza.