Jumamosi , 23rd Jun , 2018

Mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia timu ya taifa ya Ujerumani, imefufua matumaini ya kusonga mbele baada ya kushinda kwa mabao 2-1 dhidi ya timu ya taifa ya Sweden ambayo haijawahi kuwafunga kwa miaka 40.

Wachezaji wa Ujerumani kwenye mchezo dhidi ya Sweden.

Ujerumani sasa wameamka kuonekana kutaka kulinda ubingwa wao waliochukua mwaka 2014 nchini Brazil baada ya mechi ya kwanza kupoteza dhidi ya Mexico.

Ujerumani wapo kwenye hatari ya kufuata nyayo za Mabingwa wa 2010 nchi ya Hispania ambao waliondolewa hatua ya makundi nchini Brazil mwaka 2014. Ufaransa pia nao waliondolewa hatua ya makundi mwaka 2002 baada ya kushinda mwaka 1998.

Sweden ambayo ilitangulia kwa bao la mapema ilishindwa kulinda bao lake ambalo lingefuta rekodi  yao ya kutoifunga Ujerumani tangu walipoifunga 3-1 mwaka 1978. Bao la Sweden lilifungwa na Ole Ola Toivonen dakika ya 32 na marco Reus kusawazisha dakika ya 48 na Toni Kroos kuongeza dakika ya 90.

Baada ya mwaka 1978 timu hizo zimekutana mara 12 ambapo Ujerumani imeshinda mara 6 na kutoka sare mara 6.  Katika Kundi F sasa Ujerumani ina alama 3, Sweden 3 na Mexico 6 huku Korea ya Kusini wakiwa hawana alama.