Tambwe atia matumaini

Tuesday , 14th Nov , 2017

Mshambuliaji wa Yanga Amissi Tambwe amefanya mazoezi mepesi leo ikiwa ni ishara kwamba yupo mbioni kurejea kuanza kuitumikia klabu hiyo.

Yanga SC leo imefanya mazoezi kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wake ujao wa ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Mbeya City utakaopigwa Jumapili hii.

Tambwe ambaye hajacheza kabisa msimu huu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti, alikuwepo kwenye mazoezi leo ambapo amefanya mazoezi mepesi ya kukimbia pamoja na kunyoosha viungo.

Katika mazoezi ya leo kiungo Tshishimbi hakuwepo na daktari wa timu, Edward Bavu amesema kwamba mchezaji huyo anasumbuliwa na homa ya Malaria lakini anatarajia kurudi mazoezini kesho sambamba na wachezaji wengine waliokuwa na Taifa Stars nchini Benin.