Jumanne , 13th Mar , 2018

Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF leo limetangaza kuwa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 13 (U13) inatarajiwa kushiriki michuano ya vijana inayoandaliwa nchini Ubeligji.

TFF imeeleza kuwa michuano hiyo itashirikisha timu za vijana za nchi zaidi ya 10 kutoka mataifa mbalimbali na itafanyika mwezi Agosti, 2018 nchini Ubeligji.

Michuano hiyo inatarajia kukusanya timu za vijana kutoka taifa moja la bara la America ya Kusini, Asia pamoja na zingine za Ulaya huku Africa ikiwa Tanzania pekee ndio imepata mwaliko huo.

Taarifa ya TFF imeeleza kuwa michuano hiyo ni maalum kwa kuwajenga wachezaji hao kwaajili ya soka la kulipwa, ambapo wanapata fursa ya kukutana na mawakala wa wachezaji na timu mbalimbali hivyo inaweza ikafungua milango kwa vijana wa Tanzania.

Timu mbalimbali za taifa za vijana kuanzia miaka 13, 16 na 20 zipo kambini kwaajili ya michuano tofauti tofauti ambapo Serengeti Boys inajiandaa na michuano ya CECAFA kwa vijana itakayofanyika Burundi.