Jumamosi , 24th Mar , 2018

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Joyce Fissoo amewataka Watanzania kutumia vizuri fursa za masoko ya filamu kwaajili ya kujiingizia kipato kwasababu Tanzania ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa filamu Africa ikitanguliwa na Nigeria.

Akiongea kwenye kikao na wadau wa filamu mkoani Shinyanga Bi. Fissoo amesema ni lazima waigizaji watumie fursa zinazotengenezwa na Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kwenye eneo la masoko ya filamu.

''Tunapozungumzia filamu Tanzania ni ya pili baada ya Nigeria, na ukizungumzia Tanzania pia Shinyanga ipo ndani yake kwahiyo hii ni fursa kwenu ambapo bodi ya filamu na Wizara zinashirikiana kuhakikisha kazi za sanaa zinapata masoko'', amesema.

Aidha Katibu Mtendaji huyo wa bodi ameweka wazi kuwa Bodi hiyo imekuwa ikifuatilia kila hatua ya wasanii ndio mana siku za hivi karibuni ilimlipia tiketi ya ndege msanii mkongwe wa filamu Monalisa kwenda kwenye sherehe za Tuzo huko nchini Ghana.

Monalisa alichaguliwa kuwania tuzo ya mwigizaji bora wa kike Afrika kwenye tuzo za The African Prestigious Awards zinazotolewa nchini Ghana. Msanii mwingine ni Vicent Kigosi maarufu Ray ambaye naye alikuwa anawania kipengele cha mwigizaji bora wa kiume.