Jumatano , 16th Oct , 2019

Shirikisho la soka Tanzania TFF limethibitisha kuwa linatatarajia kupunguza sehemu ya wafanyakazi wake na kuunda safu mpya ili kuendana na kanuni za Shhirikisho la Soka Duniani FIFA.

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau

Hayo yamethibitishwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Wilfred Kidau katika mkutano na wanahabari leo, makao makuu ya shirikisho hilo, Ilala Jijini Dar es Salaam.

Kidau amesema kuwa hatua hiyo imekuja kutokana na taarifa ya mabadiliko ya katiba waliyopokea kutoka FIFA ya kuwataka kuunda upya Kamati za Utendaji na nafasi zingine ndani ya shirikisho hilo.

"FIFA walikuja hapa wakataka kukutana na wadau ambao mabadiliko hayo ya katiba yanawahusu. Kwenye maeneo ambayo ni ya lazima tufanye, wametaka tupunguze ukubwa wa Kamati yetu ya Utendaji", amesema Kidau.

"Wametaka tuwe na vikao vya Kamati ya Utendaji kila baada ya miezi miwili badala ya miezi mitatu. Pia wajumbe wa Kamati yetu ya Utendaji ni wengi karibia 130 wakati wenzetu Nigeria wanapigiwa kura na wajumbe 39", ameongeza.

Pia katika mabadiliko hayo ya uongozi, Wilfred Kidau amesema kuwa TFF imemteua aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura kuwa Mkurugenzi mpya wa Habari na Masoko wa shirikisho hilo.