Jumatano , 11th Jul , 2018

Viongozi wa klabu ya soka ya Mtibwa Sugar wamelazimika kusafiri kutoka Morogoro na kuja Dar es salaam, kwaajili ya kukaa meza moja na viongozi wa TFF ili kumaliza utata juu ya ushiriki wao katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika.

Maofisa wa TFF, kutoka kushoto ni Salum Madadi mkurugenzi wa ufundi, katibu mkuu wa TFF Kidao Wilfred na Afisa habari Cliford Ndimbo. (Picha haihusiani na habari)

Afisa habari wa Mtibwa Sugar Thobias Kifaru, amethibitisha hilo na kuwatoa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo kuwa, nafasi yao ya kushiriki michuano ya Kombe la shirikisho barani Afrika iko palapale kwani wako mbioni kuamaliza taratibu zote.

''Kimsingi ni suala dogo tu, ambalo lipo ndani ya uwezo wetu kwa kushirikiana na viongozi wa TFF, sisi tumeshalipa faini na kumaliza adhabu yetu lakini kwasababu viongozi hawa hawakuwa madarakani wakati huo lazima tukae nao tuongee na ndio maana viongozi wamekwenda Dar es salaam kushughulikia hilo'' - amesema.

Mwaka 2003, Mtibwa Sugar ilifungiwa na CAF kutoshiriki michuano yoyote inayosimamiwa na shirikisho hilo kwa misimu miwili, kutokana na kushindwa kwenda kucheza mechi ya marudiano dhidi ya Santos FC ya Afrika Kusini katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika. Katika mchezo wa kwanza hapa nyumbani Mtibwa Sugar ilifungwa mabao 3-0.

Kwa mujibu wa TFF, shirikisho la soka barani Afrika CAF limeitaka Mtibwa Sugar kuwasilisha ushahidi wa maandishi (stakabadhi) ya malipo ya faini ya dola 1500, walizopigwa kutokana na kosa la kutokwenda kucheza mchezo wa marudiano na endapo watakabidhi ushahidi huo kabla ya Julai 20 wataruhusiwa kushiriki msimu ujao.