Alhamisi , 3rd Dec , 2020

Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) limekemea kauli zenye lengo la kuzuia haki ya mashabiki kuingia viwanjani.

Taarifa hiyo ya TFF imesainiwa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Mario Ndimbo

Taarifa iliyotolewa na kusainiwa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Mario Ndimbo inasema,

“Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) linakemea kwa nguvu kauli zenye lengo la kuzuia haki ya washabiki kuingia viwanjani.”

Taarifa hiyo ikasisitiza kuwa, “kwa mujibu wa katiba ya shirikisho la kimataifa la mpira wa miguu FIFA na ile ya TFF, vitendo vya aina yoyote ya ubaguzi havikubaliki katika mpira wa miguu. Hivyo mshabiki yeyote anaruhusiwa kuingia kwenye mechi ya mpira wa miguu nchini ikiwa tu havunji sheria na taratibu za mpira wa miguu ambazo zimeainishwa kupitia katiba na kanuni husika''.

Taarifa hiyo ilimaliza kwa kusema, ''Hata klabu ambazo zinamiliki viwanja, hutenga tiketi maalum kwa ajili ya timu pinzani na makundi maalum.”

Taarifa hii ya TFF imekuja baada ya hapo jana Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba Haji Manara, kusema kuwa mchezo wao wa kimataifa wa klabu bingwa Afrika wa hatua ya awali wa mkondo wa pili dhidi ya Plateau United ya Nigeria, kuwa mashabiki wa klabu hiyo pekee ndio wanapaswa kuingia uwanjani kwenye mchezo huo na mashabiki wa timu nyingine tofauti na Simba SC wasijitokeze kwenye mchezo huo.

Kauli ya Manara imezua mijadala miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka wakiamini kauli hiyo inaweza, kusababisha migogoro au vurugu miongoni mwa mashabiki endapo kama mashaki tofauti na wale wa klabu ya Simba watajitokeza katika mchezo huo.