Ufaransa kutumia uzoefu kuwanyanyasa Croatia ?

Alhamisi , 12th Jul , 2018

Ufaransa ambao wameshawahi kutwaa ubingwa wa dunia mara moja, watacheza fainali ya kombe la dunia dhidi ya Croatia, taifa ambalo ndio litakuwa linacheza hatua hiyo kwa mara ya kwanza.

Bao la Mario Mandžukić (mwenye jezi nyeusi) alilofunga dakika ya 109 na kuipeleka fainali timu yake.

Hii imekuja baada ya Croatia kuwaondoa England katika mchezo wa nusu fainali kwa kipigo cha mabao 2-0, katika mchezo ambao umechezwa kwa dakika 120. Bao la Mario Mandžukić dakika ya 109 liliungana na bao la kusawazisha la Ivan Perisic la dakika ya 68 na kulipoteza bao 1 la kutangulia la England lililofungwa na Kieran Trippier.

Mchezo wa fainali sasa unakutanisha mataifa mawili yenye historia tofauti, ambapo Ufaransa wanauzoefu zaidi wa kucheza hatua ya fainali wakiwa tayari wameshacheza mwaka 1998 na kutwaa ubingwa dhidi ya Brazil huku wakipoteza fainali ya mwaka 2006 dhidi ya Italia.

Kwa upande wa Croatia wao ni wageni wa hatua hiyo wakiwa ndio wamefika kwa mara ya kwanza. Wakiwa na kizazi cha dhahabu Croatia wamekuwa na safari imara kuanzia hatua ya makundi ambapo waliongoza kundi kwa kushinda mechi zao zote ikiwemo 3-0 dhidi ya Argentina.

Nayo timu ya taifa ya England imekuwa na bahati mbaya na hatua ya nusu fainali ikiwa imeshaondolewa katika nusu fainali 4 tofauti. Ilipoteza nusu fainali ya Euro 1968 dhidi ya Yugoslavia, ikapoteza nusu fainali kombe la dunia mwaka 1990 na Euro 1996 zote dhidi ya Ujerumani pamoja na ya leo dhidi ya Croatia.