Jumanne , 16th Oct , 2018

Timu ya taifa ya Uganda imejihakikishia kwa asilimia zaidi ya 90, kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika, AFCON 2019 nchini Cameroon, baada ya kushinda mchezo wake wa 4 kwenye kundi L dhidi ya Lesotho usiku huu. Matokeo hayo yanatoa ahueni kwa Tanzania ambayo nayo imeshinda.

Mbwana Samatta akijaribu kuwatoka wachezaji wa Cape Verde.

Kimahesabu Uganda ambayo imeshinda mabao 2-0 na kufikisha alama 10, sasa inahitaji alama 1 tu ili kufuzu vinginevyo ni lazima ipoteze mechi zake mbili dhidi ya Tanzania na Cape Verde, tena kwa idadi kubwa ya mabao tofauti na hapo tunaweza kusema Uganda wamefuzu.

Kwa upande wa Tanzania ambayo imecheza nyumbani kwenye uwanja wa taifa, imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 ambayo sasa yanaifanya iwe na alama 5, ikiwa katika nafasi ya pili huku ikihitaji ushindi katika mechi zake mbili dhidi ya Lesotho na Cape Verde.

Baada ya mchezo wa leo Waziri mwenye dhamana ya Michezo, Harrison Mwakyembe, ametoa pongezi zake kwa wachezaji na mashabiki. ''Taifa Stars leo mmetupa raha watanzania, mmeitendea haki bendera ya taifa na jezi yetu na uwanja wetu, nawapongeza wachezaji na mashabiki waliokuja uwanjani leo'', amesema Mwakyembe.

Msimamo wa Kundi L sasa unaongozwa na Uganda alama 10, Tanzania alama 5, Cape Verde alama 4 na Lesotho wakiwa na alama 2 mkiani.