Alhamisi , 21st Mar , 2019

Winga wa klabu ya Difaâ Hassani El Jadidi ya Morocco na timu ya taifa ya Tanzania, Simon Msuva, amesema ushindi wa Simba unawapa hamasa zaidi ya kushinda mchezo wa Jumapili dhidi ya Uganda ili kuendelea kujitengenezea sifa katika klabu zao.

Simon Msuva (katikati)

Akiongea leo kwenye kambi ya timu ya taifa Jijini Dar es salaam, Msuva amesema wao kama wachezaji wanaocheza nje ya nchi wanapata heshima kubwa kutokana na Simba kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa ambapo hivi sasa wapo kwenye hatua ya Robo fainali.

''Taifa Stars ikishinda sisi tutaheshimika huko nje ukizingatia Simba nao wapo kwenye hatua nzuri hivyo sisi tunakuwa hatuchukuliwi poa tena, kwahiyo mchezo wa Jumapili ni muhimu sana'', amesema Msuva.

Aidha Winga huyo aliyewahi kutamba akiwa na Yanga, amewaomba mashabiki kuja uwanjani na kuwashangilia akiamini kuwa kelele zao zitawapa jukumu la kushinda na watapambana kulitimiza.

Msuva yupo kwenye msimu wake wa pili ndani ya Difaâ Hassani El Jadidi na ameshajihakikishia nafasi ya kucheza katika timu hiyo inayoshika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi kuu ya Morocco.