Ijumaa , 13th Mar , 2020

Dunia ipo katika tahadhari kubwa hivi sasa kufuatia mlipuko wa virusi vya Corona vilivyoanza mwanzoni mwa mwaka 2020 nchini China. 

Mchezo wa PSG dhidi ya Dortmund

Virusi hivyo vimeendelea kuiathiri dunia katika nyanja mbalimbali ikiwemo katika tasnia kubwa ya kimichezo, ambapo katika kipindi kifupi cha hivi karibuni, shughuli mbalimbali katika tasnia hiyo zimesimamishwa.

Katika mchezo wa mpira wa kikapu, Ligi ya Kikapu nchini Marekani NBA imesimamishwa kwa muda usiojulikana kuyokana na kuenea kwa kasi kwa virusi hivyo, huku michuano ya Formula 1 katika Australian GP ikisimamishwa baada ya mmoja wa wahusika katika timu ya McLaren kukutwa na virusi hivyo.

Shirikisho la Tennis duniani ATP, pia limethibitisha kusimamisha mashindano ya wanaume mpaka mwishoni mwa mwezi Aprili, ikenda sambamba na kusimamisha michuano hiyo katika miji ya Barcelona, Miami, Budapest, Houston na Marrakech.

Katika soka, ligi mbalimbali barani Ulaya na Amerika zimesimamishwa kwa muda ikiwemo, Ligi ya Uholanzi 'Eredivisie', ligi ya Italia 'Serie A', ligi ya Hispania 'LaLiga', ligi ya Marekani 'MLS', ligi ya Mabingwa barani Ulaya na baadhi ya michezo ya ligi ya Europa na ligi ya Uingereza 'PL'. 

Baadhi ya timu zimeathirika na virusi hivyo mpaka sasa, ambapo wachezaji wake pamoja na baadhi ya watu wa benchi la ufundi wamekutwa na virusi vivyo. Timu hizo ni Juventus, Leicester City, Arsenal, Chelsea, Manchester City na Real Madrid. Shirikisho la Soka barani Ulaya UEFA linakutana kujadili uwezekano wa kusogeza mbele michuano ya Euro na michuano ya vilabu barani Ulaya kufuatia tishio hilo.