VPL kuendelea tena leo, Azam mzigoni

Jumatatu , 22nd Feb , 2021

Klabu ya Azam 'Wanalamba lamba', wanatazamiwa kushuka dimbani saa 1:00 usiku wa leo tarehe 22 Februari 2021 kucheza dhidi ya TZ Prisons 'Wanajela jela' kwenye ligi kuu Tanzania bara mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Wacheazaji wa Azam FC, Wakipongezana baada ya kufunga moja ya bao kwenye VPL msimu huu.

Kuelekea kwenye mchezo huo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Zakaria Thabiti 'Zaka zakazi' amesema “Wachezaji wapo tayari kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Prisons, tunawaheshimu wapinzani wetu ila nasi pia tupo tayari  ili kupata matokeo chanya ndani ya uwanja”.

Mchezo huo unatazamiwa kuwa wenye upinzani mkali kutokana na mahitaji ya alama 3 kwa timu zote mbili, lakini rekodi zinaonesha tokea wawili hao wakutane Oktoba 2012 wamecheza michezo 17, Azam akishinda 8, TZ Prisons akishinda 1 na sare 8.

Mara ya mwisho Wajela jela hao kuwafunga Azam ilikuwani tarehe 14 Februari mwaka 2019 ambapo walipata ushindi wa bao 1-0 kwenye dimba la sokoine jijini Mbeya na ndiyo mchezo pekee ambao Prisons wameifunga Azam ndani ya miaka 8 iliyopita.

Licha ya rekodi hiyo ya kibabe kwa wanalamba lamba hao, lakini rekodi za michezo mitano ya mwisho ya VPL wawili hao walipokutana, Azam alipata ushindi kwenye michezo miwili pekee, sare moja na kupoteza michezo miwili jambo linaloonesha upinzani mkali wa timu hizo kwa miaka ya karibuni.

Azam ipo nafasi ya tatu, wakiwa na alama 36, alama 13 nyuma vinara, klabu ya Yanga ilhali TZ Prisons ipo nafasi ya nane wakiwa na alama zake 25.

Mchezo mwingine wa VPL utakaopigwa hii leo, ni ule utakaowakutanisha timu ya Dodoma Jiji ambayo itawakaribisha Maafande kutoka mkoani Kilimanjaro, klabu ya Polisi Tanzania mchezo utakaochezwa saa 10:00 jioni kwenye dimba la Jamhuri jijini Dodoma.