Jumamosi , 13th Oct , 2018

Mbunge wa Kigoma Mjini na mdau mkubwa wa michezo nchini Zitto Kabwe, amewatetea wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Cape Verde, kwa kusema wameumizwa na tukio la kutekwa kwa Mohammed Dewji.

Wachezaji wa Taifa Stars kushoto na Zitto Kabwe kulia

Zitto kupitia mtandao wa Twitter ameweka ujumbe huo, akitamani wachezaji hao wasingepata taarifa za kutekwa kwa mfanyabiashara huyo ambaye pia ni mdau wa michezo nchini akiwa mlezi wa Simba SC.

Mo Dewji ambaye ni mwekezaji katika klabu ya soka ya Simba akimiliki asilimia 49 ya hisa za klabu ametekwa Alhamis Oktoba 11, 2018. Hadi sasa hajapatikana.

Taifa Stars jana usiku ulifungwa mabao 3-0 na wenyeji wao Cape Verde kwenye mchezo wa tatu wa kundi L, kuwania kufuzu fainali za AFCON 2019     zitakazo fanyika nchini Cameroon.

Tanzania sasa inashika nafasi ya mwisho kwenye kundi L ikiwa na alama 2 sawa na Lesotho inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na alama 2 lakini ina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa. Uganda wapo kileleni wakifuatiwa na Cape Verde zote zikiwa na alama 4.