Jumatatu , 11th Feb , 2019

Manchester United ni moja ya vilabu ambavyo wachezaji wake wengi wa zamani wameingia kwenye fani ya ukocha huku wengi wao wakifanya vizuri na wengine kufanya vibaya kiasi cha kufukuzwa.

Moja ya majukwaa maarufu ya uwanja wa Old Trafford maarufu kama ngome ya Ferguson.

Moja ya wachezaji wa zamani wa Manchester hususani wale waliocheza kwenye 'Class of 1999' ni Gary Neville ambaye alifikia ngazi ya kuifundisha timu ya Valencia ya Hispania, lakini hakudumu sana alifukuzwa kazi kutokana na matokeo mabovu.

Mchezaji mwingine ni Ryan Giggs ambaye alianza maisha ya ukocha ndani ya Man United, akifanya kazi na Louis van Gaal lakini baada ya kutimuliwa kwa kocha huyo Giggs pia aliondoka haswa baada ya ujio wa Jose Mourinho. Kwasasa Giggs ni kocha wa timu ya taifa ya Wales.

Wakati hao wakienda kuwa makocha nyota mwingine wa Man United ambaye yupo kwenye uongozi wa soka ni Edwin van der Sar  ambaye ni Mtendaji mkuu wa klabu ya soka ya Ajax ya Uholanzi.

Mbali na hao, leo Februari 11, 2019 kiungo wa zamani wa timu hiyo Paul Scholes, ametangazwa kuwa kocha wa timu ya Oldham Athletic Club ya England kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu. Oldham inashiriki 'League Two' ya nchini humo.

Anayekamilisha orodha hiyo ya nguli wa Manchester United wanaotamba kwenye vilabu ni Ole Gunnar Solskjær ambaye anaifundisha Man United kama kocha wa muda na ameisaidia kutoka nafasi ya 8 hadi ya 4 ndani ya mechi 10.

Kwasasa Ole Gunnar anasaidiwa na nyota wengine wa timu hiyo ambao ni Mike Phelan aliyecheza miaka 1989–1994 pamoja na Michael Carrick.