Jumatatu , 21st Mei , 2018

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi William Ole Nasha, amesema Wizara yake iko mbioni kupeleka mswada Bungeni utakaotoa fursa ya kuundwa kwa bodi ya walimu itakayofanya udhibiti wa kazi za walimu nchini.

Ole Nasha ameyasema hayo Bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mariam Kisangi,​ aliyeuliza juu ya hatua gani serikali inachukua hatua gani kwa baadhi ya walimu wa shule binafsi za msingi ambao huwarundikia maswali ya kazi za nyumbani wanafunzi.

''Tunatarajia mwaka huu kupeleka muswada bungeni ili kuunda Bodi ya Walimu itakayodhibiti ubora wa walimu kwa shule zote za serikali na binafsi na hii itaondoa walimu wote ambao hawana taaluma inayokubalika'', amesema Ole Nasha.

Katika swali lake Mbunge Mariam Kisangi alieleza juu ya wanafunzi kupewa maswali 100 hadi 1,200 ya kazi za nyumbani hali inayopelekea watoto kuogopa kwenda shule kwa kutomaliza kazi hizo au kulazimika kusaidiwa na wadada wasaidizi wa kazi za ndani.

Katika hilo Ole Nasha amesema walimu wote wanaofundisha shule za binafsi na serikali ni wale tu waliothibitika kuwa na viwango vinavyohitajika hivyo baada ya mswada huo jambo hilo halitakuwepo tena.