Jumanne , 18th Jun , 2019

Baada ya mapema leo viongozi wa Yanga kuoneshwa eneo la kujenga uwanja wao huko Kigamboni na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda, uongozi wa Yanga umewaita wanachama wake.

Jengo la Yanga

Kupitia taarifa iliyotolewa usiku huu, uongozi wa klabu ya Yanga umetoa wito rasmi kwa wadau na wapenzi wa klabu hiyo ambao wangependa kufanya ukarabati wa vyumba katika Jengo la Makao makuu ya klabu hiyo lililopo mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Yanga, Dkt. Mshindo Msolla, amesema Kamati ya utendaji iliyoketi mwishoni mwa wiki imebariki kuanza kwa zoezi hilo kupitia wadau wenye mapenzi mema na klabu hiyo, ili kuwawezesha wachezaji kuishi katika jengi hilo. 

“Kwenye hafla ya Kubwa Kuliko nililieleza hili, nashukuru Kamati ya Utendaji imelipitisha, sasa rasmi tunawaalika wadau, ikiwa ni mwanachama mmoja, Tawi la Yanga, Kundi la WhatsApp au hata kampuni kufika klabuni kuanzia Alhamisi, ambapo tutakuwa tumeanisha gharama za ukarabati wa kila chumba hivyo watachagua kulingana na uwezo wao,” amesema Dkt. Msolla.

Amesema kukarabatiwa kwa vyumba katika Jengo la Yanga, kutasaidia kuondoa gharama kubwa ambazo timu hiyo imekuwa ikizitumia kwenye hoteli wakati wa kambi za mazoezi ya kawaida hasa timu inapokuwa jijini Dar es Salaam. 

“Tutatoa nafasi kwa vyumba kupewa majina ya wadau waliofanya ukarabati, mfano kama ni tawi la Makao Makuu, basi Chumba kitaitwa Makao Makuu kama watapenda, hivyo hii ni nafasi nyingine wa wadau wetu kusaidia maendeleo ya klabu yao kwa kuiepusha na gharama zinazoweza kuepukika,” alisema.

Jengo la Yanga lina jumla ya vyumba 28 pamoja na maeneo mengine muhimu ikiwemo eneo la kufanyia mazoezi ya Ndani (gym) ambayo pia inahitaji ukarabati mkubwa pamoja na kuwekwa vifaa vya kisasa.