Jumanne , 11th Jun , 2019

Siku 10 zimebakia kabla ya kuanza kwa michuano ya mataifa ya Afrika AFCON nchini Misri.

Mabingwa wa AFCON 2017, Cameroon

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imekuwa timu ya kwanza washiriki kuwasili nchini humo, ambapo imeingia mnamo Juni 8 huku ikitarajia kucheza mechi mbili za kirafiki za majaribio dhidi ya wenyeji Misri na Zimbabwe.

Katika mashindano yoyote, kunakuwa na timu ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kuleta ushindani na kuwa mabingwa kabla hata ya mashindano yenyewe. Katika michuano ya AFCON 2019 kuna timu kadhaa ambazo zinapigiwa chapuo ya kushinda ubingwa kutokana na viwango vya wachezaji wao katika ligi mbalimbali msimu huu pamoja na historia zao katika michuano iliyopita.

Misri
Wenyeji Misri wamekuwa wakipigiwa upatu kuwa wanaweza kuleta changamoto kubwa kutokana na ukweli kwamba michuano hii inafanyika katika ardhi ya nyumbani, pia kikosi chao hakina utofauti mkubwa na kile kilichocheza fainali ya AFCON iliyopita dhidi ya Cameroon, fainali ambayo walipoteza kwa mabao 2-1.

Pia kuwepo kwa wachezaji wakubwa ambao wamefanya vizuri msimu huu katika ligi mbalimbali barani Ulaya kama, Mohamed Salah ambaye ameshinda ubingwa wa Klabu Bingwa Ulaya, Mohamed Elneny ambaye amecheza fainali ya Europa League akiwa Arsenal.

Senegal
Simba hawa wa Teranga wamepangwa kundi moja na Tanzania katika michuano hiyo lakini kwa ubora, wao wako juu zaidi na ni moja ya timu inayotazamiwa kuonesha ushindani mkubwa katika michuano hiyo na hata kuibuka mabingwa. Ni kutokana na kikosi bora ilichonacho, kuanzia kwa mabeki Kalidou Koulibaly na Salif Sane hadi kwa washambuliaji, Keita Balde na Sadio Mane.

Katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi 2018, al manusura wavuke katika hatua ya 16 bora baada ya kutolewa katika makundi kwa kigezo cha mabao ya kufunga na kufungwa, ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Japan.

Nigeria & Algeria 
Timu hizi nazo zina nafasi ya kuonesha kitu kikubwa zaidi katika michuano hii, baada ya kutofanya vizuri katika michuano iliyopita ambapo hazikuishia katika hatua nzuri. kutokana na aina ya vikosi ilivyonavyo, zinaweza kufanya kitu kikubwa.

Timu zingine ambazo zinapewa nafasi ya kufanya vizuri ni pamoja na Tunisia, Congo DR, Ivory Coast, Ghana, Afrika Kusini na Morocco. Kuwepo kwa timu hizi bora hakumaanishi kuwa timu zingine haziwezi kufanya maajabu, zikiwa na maandalizi mazuri zinaweza kufanya kitu kikubwa na kushangaza ulimwengu wa soka.