Jumanne , 14th Aug , 2018

Mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho barani Afrika kati ya wenyeji, Yanga SC dhidi ya U.S.M. Alger ya Algeria utakaopigwa Jumapili Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam utaamuliwa na waamuzi kutoka nchini Namibia.

Wachezaji wa Yanga wakiwa mazoezini

Shirikisho la soka barani Afrika (CAF), limewataja waamuzi hao kuwa ni Jackson Pavaza atakayesimama katikati huku wasaidizi wake wakiwa ni namba moja Matheus Kanyanga na namba mbili David Tauhulupo Shaanika na wanatakiwa kuwasili nchini kuanzia kesho.

Yanga SC ambayo imekuwa haina safari nzuri kwenye michuano hiyo ikiwa na alama 1 tu katika mechi zake 4 ilizocheza mpaka sasa, itakuwa inasaka ushindi wa kwanza dhidi ya timu ambayo walifungua nayo hatua hiyo ya makundi na kukubali kichapo cha mabao 4-0.

Safari ya Yanga SC katika michuano hiyo ilianza kwa kuchapwa mabao 4-0 na U.S.M. Alger nchini Algeria kabla ya kuja kutoa sare ya 0-0 na Rayon jijini Dar es Salaam na baadaye kufungwa na Gor Mahia 4-0 nchini Kenya na 3-2 waliporudiana hapa nchini.

Kwenye mchezo wa Jumapili Yanga itaongezewa nguvu na wachezaji wapya waliopata leseni na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), akiwemo mshambuliaji Heritier Makambo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambaye Jumapili iliyopita alifunga bao pekee dhidi ya Mawenzi FC kwenye mechi ya kirafiki iliyopigwa mkoani Morogoro.