Jumatano , 9th Jan , 2019

Klabu ya Yanga inatarajia kucheza mchezo wake wa mwisho wa hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi 2019, leo Jumatano dhidi ya Jamhuri ya kisiwani Pemba. 

Wachezaji wa Yanga

Katika mchezo huo, Yanga itakamilisha ratiba tu na kisha kupanda boti tayari kwa kurejea Jijini Dar es salaam kutokana na kutofuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Yanga ni ya pili toka mkiani katika kundi A kwa pointi zake tatu, ikishindwa kufanya vizuri katika mechi zake tatu za awali, baada ya kushinda mechi moja pekee na kufungwa mechi mbili.

Katika kundi hilo, Azam inaongoza ikiwa na pointi saba sawa na Malindi ambazo zote zimefuzu hatua ya nusu fainali. Jamhuri ina pointi nne, Yanga ina pointi tatu na KVZ inaburuza mkia na pointi moja.

Michuano hiyo ambayo ilianza Januari Mosi mwaka huu, inazishirikisha timu tisa, tatu za Tanzania Bara na sita za Zanzibar na itahitimishwa Januari 13.