Jumapili , 16th Jan , 2022

Timu ya Wananchi Yanga SC inakibarua cha kuvunja mwiko wa kutopata ushindi katika uwanja wa Mkwakwani uwanja wa nyumbani wa Coastal Union ya Tanga. Mara ya mwisho Yanga kushinda Tanga dhidi ya Coastal kwenye ligi ilikuwa mwaka 2015.

Kikosi cha Yanga

Katika muendelezo wa raundi ya 12 ya Ligi Kuu soka Tanzania bara leo moja ya mchezo ni Coastal Union dhidi ya Yanga mchezo unaochezwa katika dimba la Mkwakwani. Ni takribani miaka 6 imepita tangu Yanga ilipopata ushindi katika uwanja huo.

Mara ya mwisho Yanga kushinda Tanga ilikuwa Februari 3, 2015 ambapo waliibuka na ushindi wa bao 1-0. Na katika michezo 4 ya Ligi ya mwisho katika dimba la Mkwakwani Yanga imefungwa mara mbili na wametoka sare mara mbili, na Msimu uliopita katika Dimba hilo Yanga ilifungwa mabao 2-1. 

Mchezo wa leo unachezwa Saa 10 Jioni, Yanga ndio vinara wa Ligi wakiwa na alama 29 na hawajapoteza mchezo hata mmoja katika michezo 11. Na wanaingia katika mchezo huu wakiwa wanawazidi Coastal Union alama 12, Coastal wapo nafasi ya 4 wakiwa na alama 12.