Jumanne , 22nd Mei , 2018

Klabu ya soka ya Yanga leo itashuka dimbani kucheza na timu ngumu zaidi kuwahi kukutana nayo katika misimu ya hivi karibuni, Mbao FC ambayo haijawahi kuifunga tangu ipande daraja mwaka 2016.

Yanga ambayo haijaonja ushindi katika mechi zake 9 zilizopita katika mashindano yote, leo itakuwa wenyeji wa Mbao FC kwenye uwanja wa taifa huku ukiwa ni mchezo wa raundi ya 28 kwa Yanga na raundi ya 29 kwa Mbao FC.

Wakai Yanga inatafuta ushindi wake wa kwanza katika mechi 9 zilizopita pia itakuwa inatafuta kuishusha Azam FC katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hivyo inahitaji ushindi ili kurudisha imani kwa mashabiki na morali kwa wachezaji.

Kwa upande wa Mbao FC ambao wao wanapigana kuhakikisha wanakwepa kushuka daraja pia watakuwa wanajitahidi kulinda heshima yao ya kutofungwa na Yanga tangu wapande ligi kuu msimu wa 2016/17.

Kwasasa Yanga inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 48, nyuma ya Azam FC yenye alama 52 na Simba yenye alama 68. Mbao FC ina alama 30 katika nafasi ya 13 ambapo inahitaji kushinda ili kuendelea kujihakikishia kusalia kwenye ligi kuu.