Jumanne , 5th Oct , 2021

Kikosi cha Mabingwa wa kombe la Ngao ya Hisani ya Jamii 2021, Klabu ya Yanga inatazamiwa kusafiri kesho Jumatano ya Oktoba 6, 2021 ikitokea Jijini Dar es Salaam nakuelekea jijini Arusha kwa ajili ya kuweka kambi ya siku 10.

Kikosi cha timu ya Yanga cha msimu wa mwaka 2021-2022.

Kambi inakuja baada ya mapumziko ya majuma mawili ya michezo ya Ligi nchini kupisha kalenda ya FIFA ya michezo ya timu za taifa kuwania kufuzu kombe la Dunia ambapo Taifa Stars itacheza na Benini Oktoba 7, 2021 kwenye dimba la Mkapa.

Kuhusu safari ya kambi hiyo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli amesema watakuwa na mchezo ya kimataifa wa kirafiki ili kuendelea kuwapa utimamu wa mwili wachezaji wao huku kocha wa kikosi hicho Mohammed Nasreddine Nabi akisema ataitumia kambi hiyo kutibu suala la wachezaji wake kuchoka kuanzia dakika za 65-70 za mchezo.

"Mchezo wa kirafiki upo wakimataifa, tunajaribu kutafuta timu kutoka kwa majirani zetu tupate mechi ya kimataifa ya kirafiki, kambi kama kambi tunahitaji utulivu, tunahitaji mazingira mazuri ambayo yatatupa nafasi ya mwalimu kufanya kila kitu anachokihitaji na benchi lake la ufundi”.

“Kwahiyo tulichagua maeneo kama matatu Zanzibar, lakini mwalimu akasema twende Arusha kwanza alafu tuna mapumziko mengine mwezi wa 11 tutakwenda Zanzibar kwa ajili ya mapumziko ya mwezi wa 11". Amesema Bumbuli.