Jumanne , 22nd Mei , 2018

Klabu ya soka ya Yanga leo imefanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbao FC na kuimaliza ukame wa ushindi kwenye timu hiyo uliodumu kwa mechi tisa tangu kocha Lwandamina aachane na timu.

Kabla ya mechi ya leo Yanga ilikuwa inapitia kipindi kigumu cha kutoonja matokeo ya ushindi, ikiambuliwa vipigo vitano na sare nne kwenye mechi hizo zilizopita katika mashindano yote.

Hata hivyo ushindi wa leo umekua wa kwanza kwenye ligi, tangu walipofungwa na Simba bao 1-0 na wakaenda mechi tatu zaidi bila ushindi wakifungwa na Prisons, Mtibwa na Mwadui FC.

Kwa ushindi wa leo, Yanga imefikisha alama 51 kwenye mechi 29 na kuendelea kuwa katika nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC yenye alama 55 na Simba yenye alama 68 kileleni.

Ligi kuu ya Tanzania yenye timu 16 sasa imebakiza raundi moja kumaliza msimu wa 2017/18 na kusubiri msimu ujao ambao utashuhudia timu 20 zikisaka ubingwa wa ligi hiyo na nafasi ya kuwakilsha nchi kimataifa.