Yanga 'yalambwa 4G' Kombe la Mapinduzi

Sunday , 8th Jan , 2017

Timu ya Yanga leo imeangukia pua baada ya kulambwa mara nne na wana lambalamba Azam FC katika michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea Zanzibar.

Yanga na Azam katika moja ya mechi za Kombe la Mapinduzi mwaka jana

Katika mchezo huo ambao ni wa mwisho katika kundi A, Azam walianza mapema kuonesha dalili za ushindi pale ambapo nahodha wao John Bocco alipofungulia bomba kwa kumalizia mpira uliotemwa na kipa wa Yanga Deo Munisi kutokana na shuti la Sure Boy, na kufanikiwa kuandika bao la pili ikiwa ni dakika ya 2 ya mchezo.

Hadi mapumziko Azam walionekana kuutawala zaidi mchezo na kumaliza kipindi cha kwanza ikiwa na umiliki wa zaidi ya asilimia 50 huku ikishindwa kutumia nafasi kadhaa za wazi ilizopata kwa ajili ya mabao zaidi.

Alikuwa ni raia wa Ghana Yahya Mohamed aliyetupia bao la pili katika dakika ya 54 kwa kichwa maridadi kilichomshinda Dida ambaye hakuwa na umakini wa kutosha huku akiwa amesogea mbele zaidi ya lango na kushuhudia kichwa kikipigwa mbele yake na kuruka bila mafanikio.

Kinda wa Azam aliyerejea kutoka Mbeya City, Joseph Mahundi anaweza kuwa ndiye aliyefunga bao bora zaidi katika michuano hii, baada ya kupokea pasi akiwa umbali wa zaidi ya mita 25 na kuachia mkwaju mkali wa mbali uliojaa kimiani moja kwa moja na kuiandikia Azam bao la tatu katika dakika ya 80.

Bao la nne limefungwa na kijana toka Medeama ya Ghana Enock Agyei baada ya kumalizia kiufundi pasi ya Afful dakika ya 85, na kufanya ubao usomeke Yanga 0-4 Azam hadi mwisho wa mchezo.

Akizungumzia mechi hiyo Abubakary Salum 'Sure Boy' kwa upande wa Azam amesema siri kubwa ya timu yao kubadilija siku ya leo tofauti na mechi zilizopita ni kuanza kuzoeana kwa wachezaji ambao wengi wao ni wageni.

Naye Saimon Msuva kwa upande wa Yanga amesema wameyapokea matokeo hayo kwa masikitiko makubwa ingawa huo ndiyo mchezo na hayo ni matokeo ya kimcheo na kwamba wanajipanga kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali.

Kwa matokeo hayo Azam wanamaliza wakiwa vinara wa kundi baada ya kukusanya point 7 wakifuatiwa na Yanga wenye point 6 na Zimamoto ina point 3.

Katika mchezo mwingine wa kundi hilo, Zimamoto imeifunga Jamhuri mabao 2-0 huku timu zote zikiaga rasmi mashindano hayo na Jamhuri inaondoka ikiwa na point moja iliyoipata katika mechi yake na Azam, lakini ikiwa haina goli hata moja na Zimamoto imeambulia point 3 ilizopata leo