Jumatatu , 16th Apr , 2018

Klabu ya Mabingwa Watetezi Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imewasili nchini Ethiopia leo hii ikiwa tayari kwa mchezo wake wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Welayta Dicha siku ya Jumatano Aprili 18, 2018.

Katika mchezo huo, Yanga itakuwa na jumla ya wachezaji 20 na viongozi 13 wakiwemo 8 wa benchi la ufundi huku ikimkosa nyota wake Ibrahim Ajib Migomba kutokana na majeruhi aliyokuwa nayo.

Mechi hiyo inatarajiwa kupigwa kwenye uwanja wa Hawassa mjini Hawassa na Yanga itakuwa na jukumu la kulinda ushindi wake wa 2-0 ilioupata kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika uwanja wa Taifa Jijini, Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.

Wachezaji waliosafiri ni Makipa Youthe Rostand na Beno Kakolanya. Mabeki Hassan Kessy, Juma Abdul, Mwinyi Haji Mngwali, Gardiel Michael, Abdallah Shaibu ‘Ninja’,  Kelvin Yondan na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavario.

Viungo ni Papy Tshishimbi, Yussuf Mhilu, Raphael Daudi, Pius Buswita, Geoffrey Mwashiuya, Said Juma ‘Makapu’, Juma Mahadhi na Emmanuel Martin wakati washambuliaji ni Obrey Chirwa, Yohana Mkomola na Thabani Kamusoko.