Yanga yatoa majibu kuhusu kumtaka Niyonzima

Ijumaa , 22nd Nov , 2019

Imefahamika kwamba mashabiki wa klabu ya soka ya Yanga ndio wanamhitaji nyota wa zamani wa klabu hiyo Haruna Niyonzima na si benchi la ufundi kama inavyoripotiwa.

Haruna Niyonzima

Akizungumza na kipindi cha Kipenga cha East Africa Radio, afisa habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema hakuna ripoti ya kocha inayoonyesha kumhitaji kiungo huyo mnyarwanda, lakini wameamua kufanyia kazi maombi ya mashabiki wao ambao wamekua wakipendekeza arejee katika dirisha dogo la usajili.

Bumbuli amesisitiza kwamba waliamua kulipeleka suala hilo katika kamati husika ambayo imekua ikifuatilia kiwango cha nyota huyo tangu katika mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars dhidi ya Rwanda, lakini pia katika michezo ya Taifa lake ya kufuzu AFCON 2021.

Kama haitoshi kamati ya ufundi inatarajiwa kuangalia kiwango cha Niyonzima katika michuano ya Cecafa Senior Challenge, inayotarajiwa kutimua vumbi  mwezi ujao kabla ya kufanya maamuzi ya kumsajili.

Niyonzima aliondoka Yanga miaka miwili iliopita na kusajiliwa na Simba kabla ya kuachwa katika usajili iliopita na kurejea nchini mwao Rwanda na mpaka sasa anakipiga na AS Kigali .