Yanga yatoa utaratibu

Jumanne , 13th Mar , 2018

Kuelekea mchezo wa marejeano wa ligi ya Mabingwa Barani Afrika kati ya wenyeji Township Rollers ya Botswana na Yanga SC, idadi ya tiketi kwa timu ngeni imetolewa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu ya Yanga ambayo kikosi chake kimeondoka nchini leo kuelekea Gaborone, imeeleza kuwa kuna jumla ya tiketi 150 ambazo mashabiki wa mabingwa hao wa soka wa Tanzania wataingia uwanjani.

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Jumamosi hii Machi 17 kwenye uwanja wa taifa wa Botswana ambao una uwezo wa kuingiza mashabiki elfu 22,000. Uwanja huo upo katikati ya jiji la Gaborone.

Kikosi cha Yanga kilichoondoka alfajiri ya leo kinaundwa na wachezaji 20  pamoja na viongozi 11 ambao wote kwa pamoja watakuwa na jukumu la kusaka ushindi wa kuanzia 2-0 au zaidi ili kupata nafasi ya kuingia hatua ya makundi.

Township Rollers ambayo ilishinda 2-1 kwenye mchezo wa kwanza, inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu ya nchini humo, ikiwa na alama 46 katika mechi 20 sawa na Yanga yenye alama 46 katika mechi 21.