Jumanne , 16th Oct , 2018

Uongozi wa klabu ya soka ya Yanga umefunguka kuhusiana na usajili wa timu yake dirisha dogo la usajili ya mwezi Disemba kwaajili ya kuimarisha kikosi kabla ya mzunguko wa pili kuanza.

Yanga ikiwa mazoezini

Katika mahojiano na www.eatv.tv, Katibu mkuu wa Yanga, Omar Kaaya amesema kuwa wao kama uongozi wa klabu hawana mamlaka rasmi ya kuamua nani anayetakiwa kusajiliwa.

Siwezi kulizungumzia hilo, liko chini ya mwalimu, ukifika muda husika ataleta majina ya wachezaji wa kuongeza au kama ataona hakuna umuhimu huo, amesema.

 “Lakini sasa ni mapema sana kulizungumzia kwasababu inategemea na ripoti ya mwalimu  itakapofika, sasahi ni mapema mno ”, ameongeza Kaaya.

Pia Katibu mkuu huyo amesema wachezaji walio majeruhi ni Juma Mahadhi pekee, Andrew Vicent ‘Dante’ na Juma Abdul wako vizuri na wanaweza kurejea dimbani muda wowote.

Yanga inatarajia kucheza na Alliance Fc ya Mwanza wikiendi hii katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara, mchezo utakaopigwa katika  uwanja wa taifa. Azam Fc inaongoza ligi mpaka sasa kwa alama 18 baada ya kushuka dimbani michezo nane huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Mtibwa Sugar kwa alama zake 17 na Yanga ikiwa katika nafasi ya tatu kwa alama 16.