Jumanne , 5th Nov , 2019

Aliyekuwa kocha mkuu wa klabu ya Yanga, Mwinyi Zahera amezungumza kufuatia kufutwa kazi ndani ya klabu hiyo hii leo.

Mwinyi Zahera

Akizungumza na EATV & Radio Digital, Zahera amesema kuwa yeye anasubiri barua atakayoandikiwa ili ajue sababu zilizopelekea uongozi kumfuta kazi ndipo ataamua vinginevyo.

"Mpaka wamefikia kufanya hivyo wana sababu, sasa hizo sababu wataniandikia kwenye barua. Na mimi nasubiri barua na mkataba wangu nijue ndipo itajulikana kama ni sheria ama la.", amesema Zahera.

"Mimi hawajanikosea siwezi kuwashtaki, hawajanikosea chochote lakini najua wamefanya hivyo wakiwa na sababu", ameongeza.

Mapema leo Novemba 5, uongozi wa Yanga ukiongozwa na Mwenyekiti Dkt. Mshindo Msolla umetangaza kuachana na kocha huyo mara moja, huku ukiliondoa na benchi lote la ufundi. Kwa kipindi kilichopo, timu itaongozwa na mchezaji na kocha wa zamani wa klabu hiyo, Boniface Mkwasa 'Master' hadi hapo uongozi utakapompata kocha mwingine.