Jumatatu , 16th Apr , 2018

Timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Zanzibar (Karume Boys), imefungiwa mwaka mmoja kushiriki michuano ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Cup U17.

Mbali na kifungo hicho lakini pia timu hiyo  imepigwa  faini ya dola za Kimarekani 15,000 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 30, kwa kosa la kupeleka wachezaji waliozidi umri.

Michuano ya CECAFA Challenge Cup U17 inaendelea nchini Burundi na Zanzibar inadaiwa kuorodhesha wachezaji waliozaliwa kabla ya Januari 1 mwaka 2002, ambao wazi wamezidi umri unaotakiwa wa miaka 17.

Kwa kifungo hicho ni wazi Karume Boys watalazimika kusubiri hadi mwaka 2020 endapo watafuzu kucheza fainali hizo kutokana na michuano hiyo kuchezwa kila baada ya miaka miwili na kifungo hicho kinafanyakazi pale timu inapofuzu.

Kwa upande wa ndugu zao vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Tanzania Bara, Serengeti Boys jana wamecheza na Uagnda na kutoa sare ya 1-1 katika mechi yake kwanza ya michuano hiyo.