Zawadi nyingine Serengeti Boys, waahidiwa magari

Jumamosi , 13th Apr , 2019

Wachezaji wa timu ya taifa ya vijana U-17 ya Tanzania, 'Serengeti Boys' wamezidi kupewa hamasa kubwa kuelekea michuano ya AFCON ya vijana inayotarajia kuanza kesho.

Serengeti Boys

Mlezi wa Timu hiyo ya vijana (Serengeti Boys), Dkt.Reginald Mengi ametembelea mazoezi ya mwisho ya timu na kuahidi kutoa Gari kwa kila mchezaji endapo timu hiyo itashinda michezo yake miwili na kufuzu fainali za Kombe la Dunia za vijana.

Pia Dkt. Mengi ameahidi kutoa milioni 5 kwa mchezaji atakayefunga bao la kwanza la timu hiyo katika mechi zake.

Serengeti Boys inatarajia kukata utepe wa mashindano hayo kwa mchezo wa ufunguzi dhidi ya Nigeria, mchezo utakaopigwa kuanzia saa 10:00 jioni huku mchezo wa pili, Angola ikitarajia kucheza na Uganda, saa 1:00 usiku.

Serengeti Boys imepangwa katika kundi A pamoja na timu za Nigeria, Angola na Uganda huku kundi B likiwa na timu za Guinea, Cameroon, Morocco na Senegal.