Zidane arejea Madrid baada ya miezi 10 kupita

Jumatatu , 11th Mar , 2019

Klabu ya soka ya Real Madrid leo Machi 11, 2019, imemfuta kazi kocha Santiago Solari na kumrejesha kocha wake wa zamani Zinedine Zidane.

Zinedine Zidane

Mabingwa hao wa kihitoria wa Ulaya wamethibitisha kurejea kwa Zidane ikiwa ni miezi 10 imepita tangu Mfaransa huyo alipotangaza kuachana na klabu hiyo Mei 31, 2018.

Zidane ambaye aliipa Madrid ubingwa wa Ulaya mara tatu mfululizo amesaini mkataba wa miaka mitatu unaomalizika mwaka 2022.

Zidane amerejea baada ya Real Madrid kupitia kipindi kigumu kwa miezi hiyo 10 ikimfukuza kocha Julen Lopetegui ambaye alichukua mikoba ya Zidane ambaye naye hakudumu katika nafasi hiyo akatimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Santiago Solari ambaye naye leo katimuliwa.

Real Madrid imetolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ajax wiki iliyopita kwa kufungwa 4-1 nyumbani. Kwenye La Liga Real ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 51 wakati vinara Barcelona wakiwa na pointi 63.

Mkataba wa Zaidane unatajwa kuwa na vipengele vyenye masharti kwa klabu ikiwemo yeye kuwa na uamzi wa mwisho ndani ya kikosi, usajili wa nyota kama Neymar, Hazard na Mbappe pamoja na ruhusa ya kuwaondoa wachezaji asiowahitaji huku Gareth Bale akitajwa kama miongoni mwa wachezaji watakaoondoka.