Alhamisi , 18th Oct , 2018

Suala la mchezaji au timu kujifunga bao ni moja kati ya vitu vibaya sana katika mchezo wa Soka.
Linapotokea tukio kama hilo, kila mmoja ni lazima atakutazama kwa namna yake, wapo watakaomtazama mchezaji kwa hasira na wapo watakaochukulia ni kawaida.

Klabu kubwa katika EPL

Zifuatazo hapa ni timu vigogo za ligi kuu soka nchini Uingereza na mabao ambayo zimejifunga mpaka sasa, katika historia ya ligi hiyo.

Everton (48), hii ni moja kati ya timu kongwe nchini Uingereza, ikiwa imeanzishwa mwaka 1888 kabla ya kugawanyika na kuunda timu mbili, nyingine ikiwa ni  Liverpool. Imejifunga jumla ya mabao 48 mpaka sasa katika historia ya ligi hiyo, ambapo mabao 6 kati ya hayo yakichangiwa na mlinzi Phil Jagielka.

Arsenal na Liverpool (39), timu hizi zinakamata namba tatu katika listi ya klabu zote zilizojifunga mabao mengi mpaka sasa kwenye historia ya EPL, zikiwa ni za pili katika listi ya vigogo waliojifunga mabao mengi. Mmoja wapo anaweza kuongeza idadi ya mabao hayo msimu huu.

Manchester City (37), Manchester City ya sasa ni tofauti na ya miaka kadhaa iliyopita, ilikuwa ni klabu ya kawaida ambayo haikuwa hata katika listi ya timu zinazohesabiwa katika kuwania taji la ligi, lakini sasa imeweza kuhimili makosa ya kutojifunga na kuwa moja ya klabu kubwa, bora na yenye mafanikio.

Manchester United (36), mashetani hao wekundu wanashika nafasi ya nne katika listi ya vigogo na nafasi ya nane katika listi nzima ya klabu zilizojifunga mabao mengi mpaka sasa, mabao 5 kati ya hayo 36 yakichangiwa na mlinzi mstaafu wa timu hiyo, Rio Ferdinand.

Chelsea (34), kabla ya bilionea, Roman Abramovic kuinunua klabu hiyo na kuifanya kuwa moja ya klabu kubwa na tajiri, mambo hayakuwa mazuri sana kiasi cha kuruhusu idadi hiyo ya mabao ya kujifunga.