Jumatano , 25th Jul , 2018

Msanii wa Bongo fleva anayetamba na ngoma yake mpya ya ‘totoa’ Aslay Isihaka amefunguka kuwa kufanya kazi nje ya kundi hakumpi ugumu wowote kwani kuvunjika kwa Yamoto Band hakuna aliyepanga.

Msanii wa Bongo fleva, Aslay Isihaka.

Aslay amesema hayo kupitia KIKAANGONI ya East Africa Television, inayorushwa mubashara kwenye ukurasa wake wa Facebook, ambapo amefunguka kuwa ameanza safari ya muziki mwenyewe na hata ilipotokea nafasi ya kuingia kwenye kundi haikuwa na ugumu wowote kwakuwa aliamini katika bidii yake.

Kutokuendelea kwa kundi letu yawezekana kwamba Mungu hakupenda ndiyo maana hatukuweka hata kikao cha kuvunja kundi, ilitokea tu na kila mmoja akaanza kutoa wimbo wake binafsi kwa muda mfupi na mimi ndio nilianza kutoa nyimbo”, amesema Aslay.

Aslay amefunguka pia kuhusiana na tetesi kuwa alikuwa akipendelewa ndani ya Yamoto, ambapo amesema kuwa kila mtu alikuwa anapatiwa sawa, ingawa kuna vitu alikuwa akipata kama kiongozi lakini siyo kwamba ni kutokana na upendeleo.

Kundi hilo lilitambulishwa rasmi katika ulimwengu wa sanaa ya muziki wa kizazi kipya, mwaka 2014 na kufanya kazi kadhaa zilizotamba ikiwemo ‘Nitajuta na Nisambazie raha’, lilivunjika mwaka 2017 baada ya kinachodaiwa kuwa ni mgawanyiko ndani ya bendi hiyo.