Jumanne , 14th Feb , 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameshuhudia Utiaji Saini wa Mikataba ya Utekelezaji wa Miradi Mahsusi ya Umeme leo tarehe 14 Februari, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam

Akizungumza baada ya utiaji saini huo Rais Samia amesema jumla ya mikataba 26 imesainiwa leo

"Leo tumesaini mikataba ya Trilioni 1.9 kwa ujumla ambayo ni mikataba 26, lakini pia tumesaini pia mikataba ya kupeleka umeme kwenye migodi midogo midogo, maeneo ya kilimo, vituo vya afya, viwanda vidogo na vyanzo vya maji" amesema Rais Samia

Rais Samia amesema kuwa kwenye sekta ya migodi umeme un akwenda kuwa msaada mkubwa kwa wachimbaji wadogo wadogo katika kazi zao

"Tukipeleka umeme kwenye migodi kama mlivyoona hali yao sio nzuri sana lakini ukipeleka umeme wa kutosha hata zile mashine wanazotumia na mitambo wanayotumia kuchimba itabadilika"

Aidha Rais Samia amekemea tabia ya baadhi ya viongozi kuwaandaa wakandarasi wao kwa ajili ya kupewa miradi na wanapokosa wanakwenda kushitaki na kusimamisha miradi hiyo jambo ambalo amesema linarudisha nyuma maendeleo

"Natambua kuna wenzetu wengi ambao kila mtu alikuwa na mkandarasi wake mkononi na alipenda apate, na kwasababu hakupata fitina ni nyingi, mbio PPRA, mbio PCCB, mbio sjui wapi, ule mradi usifanyika kwa matakwa yake binafsi, hatutakwenda hivyo"

"Ili miradi hii ifanyike haraka ili tupate maendeleo ya haraka tunahitaji maamuzi ya haraka, unapokosa ukaenda PCCB, PPRA na kwingine unazuia miradi kufanyika, unazuia utendaji kwenda kwa haraka, na wenye taasisi hizi pimeni mnacholetewa"