Monday , 27th Mar , 2017

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Nchemba amewataka maafisa wa jeshi hilo kutenda haki kutokana na baadhi yao kunyooshewa vidole kwa kukiuka misingi ya kazi zao ikiwamo kujihusisha na rushwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba (kulia) akitoa hotuba ufunguzi wa kikao kazi cha mwaka kinachowahusisha maafisa wakuu wa jeshi la Polisi na makamanda wa mikoa na vikosi kinachofanyika mkoani Dodoma.

"Sisi tupo kwa ajiliI ya kuwasaidia wananchi na hata mheshimiwa Rais tangu anafanya kampeni ajenda yake ilikuwa ni kuwasaidia wanyonge, tukumbuke sisi tupo kwa ajili ya haki na siyo kuvunja misingi hiyo, sasa wengine wapo kwa ajili ya kubadilisha kesi, akiomba rushwa akikataliwa anaamua kumbambikia mtu kesi au kumbadilishia kesi naomba muache"- Waziri alisema.

Waziri Nchemba pia amelitaka jeshi hilo kuhakikisha linaendelea na mapambano dhidi ya vitendo vya uhalifu ikiwamo vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya huku akiahidi dhamira ya serikali katika kuongeza maslahi ya askari polisi nchini pamoja na miundombinu ya makazi yao. 

Ametoa agizo hilo katika kikao cha kazi kilichoongozwa na mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Ernest Mangu na kuhudhuriwa na maafisa waandamizi, makamanda wa mikoa na wakuu wa vikosi vya polisi nchi nzima ambapo pamoja na mambo mengine kinajadili mikakati ya kukabiliana na uhalifu nchini. 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba (kulia) akiongea na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Ernest Mangu wakati wa hafla ya ufunguzi wa kikao kazi cha maafisa wakuu wa jeshi la Polisi na makamanda wa mikoa na vikosi kinachofanyika mkoani Dodoma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Waziri Nchemba amesema serikali itaendeleza jitihada zake za kuwakomboa askari katika kuongeza maslahi yao pamoja na kuboresha miundombinu ya askari

Kwa upande wake mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Ernest Mangu amesema mapambano dhidi ya madawa ya kulevya imekuwa ni tatizo sugu nchini na kuitaka jamii kutofumbia macho vitendo hivyo vya kihalifu.

Baadhi ya maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi wakiimba wimbo wa maadili ya afisa wa polisi wakati wa hafla ya ufunguzi wa kikao kazi cha maafisa hao na  makamanda wa mikoa na vikosi kinachofanyika mkoani Dodoma