Wednesday , 19th Oct , 2016

Mahakama ya Ilala Dar es salaam imemfutia shtaka la unyang’anyi kwa kutumia silaha linalomkabili mshtakiwa Salum Njwete maarufu kwa jina la ‘Scorpion’ anayetuhumiwa kumchoma kisu na kumtoboa macho, Saidi Mrisho.

Mtuhumiwa Salum Njwete (Scorpion) aliyevaa baraghashia

Awali kabla ya kusomewa shitaka hilo upande mashitaka uliiomba mahakama kuliondoa shitaka la unyanganyi wa kutumia silaha linalomkabili Salum Njwete kwa nia ya kutotaka kuendelea na kesi hiyo .

Kutokana na ombi hilo hakimu anayesimamia kesi hiyo Adelf Sachole alikubaliana na ombi hilo kuliondoa shitaka hilo kwa kuzingatia kifungu cha 91 (1) ambacho kinampa mamlaka mkurugenzi wa mashitaka (DPP) kuondoa mashitaka muda wowote ilimradi kesi hiyo isiwe imetolewa hukumu.

Baada ya saa kadhaa hakimu mwingine Frola Haule alifungua shitaka hilohilo la unyang’anyi kwa kutumia silaha linalomkabili Njwete kosa analodaiwa kulitenda mnamo Septemba 6 2016 katika eneo la Buguruni Sheli Dar es salaam pamoja na kudaiwa kuiba vitu pamoja na fedha taslimu vyote vikiwa na thamani ya shilingi 476,000 mali ya Said Mrisho

Njwete amekana mashitaka hayo na kesi hiyo imeahirishwa mpaka itakapotajwa tena Novemba 2, 2016, mshitakia amerudishwa rumande kutokana na shitaka linalomkabili kisheria kukosa dhamana.