Tuesday , 18th Oct , 2016

Rais wa Chama cha walimu nchini Gratian Mukoba amesema serikali inatakiwa ijibu madai ya malimbikizo ya walimu kwa sasa kuliko kutulia kimya wakati zoezi la uhakiki lililotangazwa na serikali likiwa limeshakamilika.

Rais wa CWT Gratian Mukoba

Mukoba ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kipindi cha East Africa Breakfast alipokuwa akifafanua siku 15 ambazo amezitangaza kwa serikali kutoa tamko la ni lini madeni yao yatalipwa.

“Hatuoni zoezi la kulipwa likiendelea wakati tuliambiwa tusubiri zoezi la uhakiki ndani ya miezi miwili likamilike kwanza, zoezi limeisha hadi sasa serikali haisemi kitu gani kinaendelea hivyo kama serikali haitajitokeza tutaanza uhamasishaji wa mgomo” Amesema Mukoba.

Mukoba ameongeza kuwa wapo walimu wamestaafu yapata miezi zaidi ya mitano lakini hawapati stahiki zao jambo ambalo linatia wasiwasi juu ya namna serikali inavyoshughulikia mambo yao.

“Pesa za walimu zinapitia PSPF hivyo sielewi kwa nini serikali haijitokezi hadharani na kuzungumza ni lini malimbikizo ya walimu yanalipwa” Amesema Mukoba.

Mukoba ameongeza kuwa wao kama chama cha walimu hawapendi kusumbuana na serikali ya Rais Dkt. Magufuli katika kuwalipa walimu kama walivyofanya katika serikali zilizopita hivyo ana imani serikali itashughulikia madeni yao kwa wakati