Tuesday , 18th Oct , 2016

Michuano ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea tena hapo kesho (JUmatano) kwa michezo sita kupigwa katika viwanja mbalimbali hapa nchini huku mchezo mmoja ukipigwa siku ya Alhamis.

Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao

Afisa Habari wa Azam FC Jaffary Iddy ambao hapo kesho wanatarajia kuikaribisha Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Chamazi Complex amesema, wamejipanga kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa saa moja jioni lengo likiwa ni kupambana ii kupata pointi tatu zitakazowaweka katika nafasi nzuri ndani ya Ligi Kuu.

Jaffary amesema, kwa mujibu wa Bodi ya Ligi wamepanga michezo yote ya Azam FC inakuwa ikichezwa saa moja jioni na siyo saa kumi jioni kama ilivyozoeleka hapo awali.

Kwa upande wake Kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar Zubeiry Katwila amesema, wanafurahia ushindani uliopo ndani ya Ligi Kuu na kwamba wamejipanga kwa ajili ya kupambana dhidi ya Azam FC hapo kesho huku akiongeza kuwa muda uliopangwa kwa ajili ya mchezo huo hauwezi kuwazuia kupata matokeo mazuri.

Naye nahodha wa Mtibwa Sugar Shaaban Nditi amesema, hawajajipanga kwa ajili ya mchezo huo pekee bali wamejipanga kupambana kwa michezo yote ya Ligi Kuu ili kuweza kuwa katika nafasi nzuri ndani ya Ligi.

Michezo mingine itakayopigwa hapo kesho ni Yanga ikiwa ugenini jijini Mwanza dhidi ya Toto African, African Lyon itaikaribisha Majimaji katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam, Ruvu Shooting wataikaribisha Mwadui kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, Ndanda itaikaribisha Mbeya City katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mjini Mtwara, Tanzania Prisons ikicheza dhidi ya Stand kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya huku siku ya Alhamis Simba SC akiikaribisha Mbao FC katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Ramadhani Singano 'Messi' akimtoka mchezaji wa Mtibwa Sugar wakati wa mchezo wao wa ligi